Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Monday, February 25, 2013

Kuhusu Wimbo wa MwanaFA uliokuwa utoke leo


                                                             TAARIFA KWA WADAU
Leo tarehe 25 Februari mwaka 2013 ndio ilikuwa iwe siku nyingine ya kihistoria katika medani ya muziki wa kizazi kipya.

Kwa siku kadhaa sasa tumekuwa tukitangaza kwamba wimbo mpya wa MwanaFA ulio katika mahadhi ya Hip Hop uitwao “Kama Zamani” aliowashirikisha Man'dojo, Domokaya na The Kilimanjaro Band (Wana Njenje) ungeanza kuuzwa kupitia njia mbalimbali kama ‘iTunes’, ‘Amazon’ na kupitia katika simu za mkononi.

Pia ndio tarehe ambayo Kama Zamani ingeanza kusikika katika vituo vya redio Tanzania na nchi za jirani.
 
Lifeline Music Inc. ndiyo inayosimamia muziki wa MwanaFA kwa sasa, ikiwa ni kampuni ambayo inafanya kazi za muziki, kuangalia na kuhakikisha kwamba wasanii inaowasimamia wananufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na kazi zao; na kwamba muziki unaofanyika kwa sasa unafuata kanuni zote zinazosimamia makubaliano ya biashara.

Kama mjuavyo, biashara yoyote ina pande mbili na mafanikio yake yanategemea zaidi maridhiano baina ya pande hizo na utimizaji wa vipengele tofauti ndani ya mikataba ya biashara.
Katika kuboresha maslahi ya wanamuziki husika na wimbo huu,pia kuboresha zaidi njia zitakazotumika kuhakikisha ya kwamba burudani hii itawafikia washabiki wengi zaidi wa muziki unaofanywa na MwanaFA, Kilimanjaro Band(Wana Njenje) na Man’Dojo na Domokaya, tumefikia uamuzi wa kusubiri na kusogeza mbele siku ya kuachia wimbo wa Kama  Zamani kama ilivyopangwa hapo awali.

Tunachukua nafasi hii kuwaomba radhi mashabiki ambao mmekuwa mnasubiri kwa hamu kusikia ni nini muungano huu wa muziki wa kizazi kipya na moja ya bendi kongwe kabisa za muziki yenye miaka zaidi ya 40 katika tasnia ya muziki Tanzania umewaandalia.

Kwa niaba ya MwanaFA, uongozi wa Lifeline Music Inc. unaomba uvumilivu na subira toka kwenu mashabiki na wapenzi wa muziki. Tunaamini kwamba subira huvuta heri na mambo mazuri hayahitaji haraka.
 
Tunawashukuru kwa dhati kwa ushirikiano wenu.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...