Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Friday, January 9, 2015

Bondia mtanzania Omari Kimweri anayetesa Australia kutoa sapoti ya mafunzo ya ndondi Dar



Omari Kimweri

.Kutua Februari, apania kuzalisha akina Mayweather kibao nchini

NA Mwandishi wetu

NDONDI ni miongoni mwa michezo maarufu mno hapa Tanzania na duniani kwa ujumla.

Wapo wanamichezo waliojipatia heshima kubwa duniani kutokana na kufanikiwa kupitia mchezo wa ndondi.

Miongoni mwa wanamichezo hao ni nguli Mohammed Ali, Mike ‘Iron’ Tyson, Evender Holyfield, Floyd Mayweather, Manny Pacquiao na wengineo wengi.

Kwa hapa nchini, wapo mabondia waliojitengenezea majina wakiwamo Emmanuel Mlundwa, Habibu Kinyogoli 'Masta' Michael Yombayomba, Stanley Mabesi 'Ninja' Rashid Matumla, Ibrahimu Class 'King Class Mawe'  na wengineo wengi.

Lakini ikumbukwe kuwa ndondi ndio mchezo uliotoa mwanamichezo anayelipwa zaidi duniani kwa sasa ambaye si mwingine bali ni Mayweather, akifuatiwa na mwanasoka raia wa Ureno anayekipiga katika klabu ya Real Madrid ya Hispania, Cristiano Ronaldo.

Anayeshika nafasi ya tatu ni mchezaji wa mpira wa kikapu LeBron James, wakati mwanasoka anayechezea Barcelona ya Hispania, Muargentina Lionel Messi akishika nafasi ya nne, huku wa tano akiwa ni mkali wa mpira wa kikapu, Kobe Bryant.

Pamoja na mafanikio hayo katika ndondi, Tanzania imeonekana kuzidi kulala usingizi wa pono katika suala zima la kuvumbua na kuendeleza vipaji vya mchezo huo kama sehemu ya kutatua tatizo sugu la ajira linaloitesa nchi yetu kwa sasa.

Unapopita huko mitaani, unaweza kukutana na vijana wadogo wakiwa wanafanya mazoezi ya ngumi kwa kutumia vifaa visivyo rasmi ambavyo mwisho wa siku, huishia kuwadumaza badala ya kuwajenga kama walivyotarajiwa.

Hali hiyo imetokana na kukosekana kwa vifaa vya kujifunzia mchezo huo, zikiwamo kumbi na hata wataalam wa kuwapa ujuzi wa kuwawezesha kufikia mafanikioi ya akina Mayweather.

Ni kwa kufahamu hilo, wapo wadau wa ndondi ambao wamekuwa wakijitoa kusaidia vipaji vya ndondi hapa nchini, miongoni mwao akiwa ni Kocha wa Kimataifa wa Ndondi nchini, Rajabu Mhamila ‘Super D’.

Bondia huyo wa zamani, ameshawahi kufanya jitihada kadha wa kadha kuendeleza ndondi hapa nchini, ikiwamo kutoa mafunzo kwa vijana chini ya klabu yake ya Ashanti Boxing Club na kupitia DVD zake zenye mapambano makali yaliyowahi kufanyika hapa nchini na duniani kwa ujumla, yakiwahusisha mabondia nyota.

Katika kuonyesha jinsi anavyoguswa na ndondi, Februari mwaka huu Super D atakuwa na ugeni mkubwa wa bondia Mtanzania anayefanya kazi zake nchini Deer Park, Victoria, Australia, Omari Kimweri ambaye anatua nchini kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wanamasumbwi wa Tanzania.

Akizungumza Dar es salaam jana, Super D anasema kuwa ujio wa Kimweri ni fursa nyingine adimu kwa mabondia wa Tanzania katika kuona ni vipi wanaweza kutimiza ndoto zao za kutoka kimaisha kupitia mchezo huo.

Anasema kuwa Kimweri atatua akiwa na vifaa mbalimbali vya masumbwi ambapo pia atatoa mafunzo na mbinu mpya zinazotumiwa na mabondia wa nje kwa mabondia pamoja na kushuhudia mapambano kadhaa yatakayofanyika kwa kipindi atakachokuwapo hapa nchini.

“Kimweri anakuja akiwa na msafara wa watu kadhaa, akiwamo mwanasoka wa kike, Melanie Gines ambaye ni raia wa Hispania. Akiwa hapa nchini, Melanie atapata fursa ya kukutana na wanasoka wa kike wa hapa , kwani amechezea timu nyingi za Ulaya,  Hispania,” anasema Super D.

Anasema kuwa ujio wa Kimweri umewezeshwa kwa kiasi kikubwa na promota wake, Brian Amatruda ambaye ni miongoni mwa mapromota maarufu nchini kwao Australia, akiwa amekubali kutoa baadhi ya vifaa vya kisasa kutoka Hispania na Marekani kwa ajili ya ziara hiyo.

Super D anasema kuwa Kimweri ambaye ni bingwa wa WBO, atatua nchini akiwa na mikanda yake yote aliyowahi kutwaa, ukiwamo wa ubingwa wa Australia, lengo likiwa ni kuwahamasisha vijana wa kitanzania kujikita zaidi katika ndondi.

“Nimezungumza na Kimweri na ameonyesha kuwa na uchungu wa kuwainua mabondia wa hapa nchini ili waweze kutimiza ndoto zao na anafanya hivyo chini ya mradi wake wa ‘Kimweri Project’ na atakuwa hapa nchini kwa wiki moja,” anasema.

Anasema kuwa ujio wa bondia huyo uliochagizwa na Super D Boxing Coach and Promotion, umelenga kuwahamasiaha mabondia kucheza mara kwa mara ili kupandisha viwango vyao kwani hiyo ndio siri ya mafanikio ya wanamasumbwi wengi duniani.


Mbali ya mafunzo kutoka kwa Kimweri, pia katika ziara zake zote sehemu mbalimbali nchini, kutakuwa na uuzwaji wa DVD za Super D zenye lengo la kutoa mafunzo kupitia mapambano ya mabondia maarufu duniani, akiwamo Floyd Mayweather,Manny Paquaio, Mohamerd Alli, na wa hapa nchini kama Mbwana Matumla, Francis

Miyeyusho,Ibrahimu Class' King Class Mawe' ambaye ni bingwa wa WPBF Africa na wengineo.
OMARI KIMWERI
bondia  Omari Kimweri ambaye ni bingwa wa uzito wa flyweight nchini Deer Park, Victoria, Australia anatalajia kucheza mpambano wake mwingine march 13 mpambano utakaopigwa katika ukumbi wa
The Melbourne Pavilion, Flemington, Victoria, Australia

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...