Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Monday, January 25, 2016

Wauzaji bidhaa holela soko la Buguruni wapigwa marufuku



Na Jacquiline Mrisho MAELEZO

Halmashauri ya Manispaa ya Ilala yapiga marufuku uuzwaji holela wa bidhaa katika soko la Buguruni unaochafua mazingira ya soko na kuhatarisha afya za walaji.

Hayo yamesemwa leo na Afisa Habari wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala David Langa wakati akifafanua kuhusu kero ya wauzaji holela wanaopanga bidhaa chini katika soko la Buguruni.

“Bidhaa zinazopangwa chini katika soko la Buguruni sio rasmi na hakuna utaratibu unaoruhusu wauzaji kufanya biashara hiyo, hivyo natoa tahadhari kwa wale wote wenye tabia hiyo kuwa ni marufuku kufanya biashara ya kupanga bidhaa chini na sio kwa soko la Buguruni tu ila katika masoko yote yaliyopo katika manispaa yetu” Alisema Langa

Afisa langa amesema kuwa wapo maaskari wanaolinda na kuthibiti uuzwaji holela wa bidhaa katika soko hilo ila wauzaji wamekuwa wakifanya mchezo wa kuwavizia maaskari pindi wanapoondoka ndipo wanapanga bidhaa zao.

Ameongeza kuwa suala hili limekuwa sugu katika masoko mengi na njia ya kukabiliana na changamoto hii ni kuongeza askari wengi watakaokaa muda wote ili waweze kukabiliana na wauzaji holela.

Aidha Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kwa kushirikiana na Maafisa Afya inafatilia kwa karibu masoko yote ili kufatilia kama wauzaji wanazingatia kanuni za afya kwa kuweka mazingira safi ili kuokoa afya za walaji.

Uchafu wa mazingira katika masoko ya Jiji la Dar es Salaam umekithiri na imekuwa ni tatizo sugu lakini Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imejipanga kupambana nalo ili kuondoa uwezekano wa kutokea kwa magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...